Sadaka 3 Unazohitaji Kufanya Ili Kutokomeza Umaskini
Nilipomfahamu mwandishi Brian Tracy na nikapenda mafundisho yake. Nilianza kutumia masaa mengi ya usiku nikimsikiliza Tracy na kusoma nukuu zake. Sentensi moja ilinigusa kutoka kwa Tracy na hiyo ni; “ikiwa unataka kufanikisha kitu tofauti, lazima ufanye kitu tofauti. Ikiwa unataka kufanikisha kile ambacho hujawahi kufanikisha, lazima ufanye kile ambacho hujawahi kufanya hapo awali.” Nilipokuwa nikikua, niliandika sentensi hiyo kwenye diary na kila siku nilipoona maneno hayo, nilijua kwamba nilipaswa kulipa gharama. Ni rahisi sana; ikiwa maisha yako si yale unayotaka kuwa sasa hivi, lazima uwe tayari kufanya kitu tofauti, vinginevyo hutoweza huhama kutoka ulimwengu mmoja rahisi kwenda mwingine. Kufanya kitu tofauti kunamaanisha kutoka nje ya eneo lako la faraja na hili halitakuwa rahisi kamwe.
Tengeneza Muda wa Kujisomea: Wakati marafiki na jamaa zangu wengi wanajua kile nilichofanikiwa na maisha yangu leo, ni rahisi kwao kunionea wivu. Miaka michache iliyopita, nilikuwa mmoja wa vijana ambao maisha yao yalikuwa janga. Nilichukia maisha yangu na nilitamani nisingezaliwa kwa sababu nilikuwa katika umaskini, na vikwazo vingine vingi. Kwa hivyo, niliwezaje kubadilisha maisha yangu, kutoka kuwa kijana aliyekuwa akichukia maisha hadi kufikia ahueni ya maisha bora kabisa kwa ajili yangu? Vitabu! Vitabu!! Vitabu!!! Maisha yangu yalibadilika siku nilipoanza kusoma vitabu na nitafafanua jinsi ilivyotokea. Kwanza, nilipoanza kusoma vitabu, nilianza kusoma hadithi za watu wa kawaida ambao walifanikisha mambo ya ajabu. Hadithi hizi zilinipa moyo na kunipa matumaini kwamba ningeweza pia kushinda kila kikwazo njiani mwangu na kufanikisha malengo ya maisha yangu.
Nafikiri hili ni rahisi sana; ikiwa unajua kwamba baadhi ya watu wana baadhi ya vikwazo unavyofikiri unavyo, lakini bado walifanikiwa, utaanza kujiamini ghafla. Unapoanza kujiamini, unaanza kufikiria makubwa na unapoongeza ukubwa wa ndoto zako, unaongeza moja kwa moja kile kinachowezekana na maisha yako. Katika kesi yangu, nilianza kuamini kwamba ningeweza kuwa tajiri, ingawa nilikulia katika kijiji maskini. Nilianza kuamini kwamba ningeweza kuwa milionea na imani hii iliniongoza kwenye kitu muhimu sana; nilianza kutafuta jinsi ya kufanikisha kile nilichoamini ningeweza kufanikisha kwa kusoma vitabu vilivyoandikwa na watu ambao wamepata pesa nyingi hapo awali. Nilianza kujifunza mawazo na vitendo vya watu hawa na kadiri nilivyowaiga watu hawa, ndivyo maisha yangu ya kifedha yalivyokuwa bora. Ndiyo, ilichukua miaka zaidi ya 4 kabla maisha yangu ya kifedha kuanza kubadilika sana, bila kusoma vitabu, nisingeweza kufanikisha.
Jambo lingine unaloweza kufanya pamoja na kusoma vitabu ni kutazama video zinazohadithia hadithi za watu waliofanikiwa. Ndiyo, vitabu ni vya kuchosha lakini ndivyo kila kitu chenye maana kilivyo. Matunda ni ya kuchosha na mboga ni za kuchosha lakini ikiwa unataka kuwa na afya utakula zaidi. Vinywaji vya soda ni vya kufurahisha, sukari ni tamu na vyakula vya haraka ni vizuri lakini ikiwa unapenda afya yako, utakimbia mbali navyo. TV ni ya kufurahisha na mitandao ya kijamii ni ya kuvutia lakini ikiwa unataka kuepuka umaskini, utatumia muda mwingi na vitabu vyako. Muda fulani uliopita, nilijua kwamba Bill Gates anasoma kitabu kimoja kila wiki. Nimesoma pia kuhusu ukweli kwamba milionea wa kawaida husoma kitabu kimoja kila wiki. Ikiwa milionea wa kawaida hufanya kitu, basi ni jambo zuri kuiga kwa hivyo niliamua kwamba nitakuwa ninasoma kitabu kimoja kila wiki. Hili si rahisi na sikuombi uanze kusoma kitabu kwa wiki. Lakini lazima ukubali kujitoa sadaka katika kusoma vitabu kama kweli unataka kuepuka na kuutokomeza umaskini katika maisha yako na familia yako.
Epuka Visingizio: Nilikuambia awali kwamba sukari ni tamu na unakubali kwamba dawa za kulevya, vyakula vya haraka, na vitu vingine vingi vya kudhuru ni vya kufurahisha. Jambo lingine tamu sana ni visingizio na ndiyo maana watu wengi hufanya hivyo. Sikiliza, unaweza kutoa sababu mia moja kwa nini uko ulipo ikiwa unataka na unaweza pia kutoa sababu moja kwa nini unahitaji kuwa mahali pengine. Tofauti ni katika jinsi unavyotumia hii mashine yenye nguvu uliyopewa na Mungu. Mashine hiyo ni ubongo wako. Kama utatengeneza mazingira ya ubongo wako kutafuta sababu kwa nini wewe ni maskini, mfumo wako wa ubongo utakuwa busy kutafuta sababu na utaanza kuona jinsi uchumi, serikali, na wazazi wako wanavyokufanya uwe maskini. Ubongo wako utaonyesha kwa haraka jinsi ukosefu wako wa elimu, changamoto yako ya afya, utoto wako au hata nchi uliyokulia ni sababu za wewe kuwa maskini. Lanikini ikiwa utatengeneza mazingira ya ubongo wako kutafuta kwa nini lazima uwe tajiri, utaanza kuona kwamba hata katika uchumi mbaya, baadhi ya watu wanapata maelfu ya dola katika biashara halali. Utaanza kusoma kuhusu watu ambao walipitia shida kama zako na walifanikiwa. Utaanza kuona kwamba una nguvu nyingi juu ya maisha yako kuliko unavyofikiria na utaanza kuchukua majukumu. Visingizio ni chakula cha wapumbavu na dunia yetu imejaa wengi wao kwa sababu Visingizio ni tamu. Ni rahisi. Kila mtu anaweza kufanya hivyo lakini ikiwa unataka kuepuka umaskini, hutaendekeza visingizio kamwe. Epuka visingizio mara zote. Tambua unachopaswa kufanya kubadilisha maisha yako na ukifanye, bila kujali jinsi ilivyo ngumu.
Badilisha Kushindwa kwa Mafanikio: Nilisikia kitu cha kuvutia sana kutoka kwa Mark Cuban siku chache zilizopita na kinanipa maana kubwa kwangu. Cuban alisema, “Haijalishi ni mara ngapi unashindwa, kumbuka unahitaji kufanikiwa mara moja tu.” Kauli hii inanipa maana kubwa kwangu kwa sababu kila ninapokumbuka miaka yangu ya kushindwa, naweza kuona maana ya kauli hii. Katika miaka yangu ya kushindwa, kila kitu nilichojaribu kilishindwa na kila mtu alifikiri nilikuwa mjinga. Nilikuwa maskini, nikakataliwa na nikakata tamaa lakini siku moja ilifika nilipopata mafanikio yangu ya kwanza. Kutoka hapo, nilipata mafanikio yangu ya pili na ya tatu. Leo, inaonekana kama kila kitu ninachogusa kinakuwa na mafanikio lakini hiyo ni kinyume na aina ya maisha niliyokuwa nayo miaka michache tu iliyopita. Hivyo, hata wewe “haijalishi ni mara ngapi unashindwa, kumbuka unahitaji kufanikiwa mara moja tu na hiyo mara moja itazima maumivu yote ya miaka ya kushindwa.” Kwanini ni muhimu uelewe hili? Watu wengi wanaona kushindwa kama jambo baya na ndiyo maana wanakata tamaa. Ikiwa unatafuta mafanikio, unapaswa kuelewa kwamba barabara inayofikisha watu kwenye mafanikio inaitwa kushindwa na kushindwa si mwisho kwa sababu mafanikio ya siku moja yanaweza kukufanya usahau maumivu ya miaka kumi ya kushindwa. Kubali kulipa gharama katika kujaribu mambo. Thubutu kutoka nje ya eneo lako la faraja. Kuwa na ujasiri wa kufanya mambo ambayo ni hatari na unaposhindwa, kuwa na ujasiri kusimama na kujaribu tena kwa sababu haijalishi ni mara ngapi unashindwa, unahitaji kufanikiwa mara moja tu.
Jambo Muhimu Zaidi katika Makala Hii ni Hili: Ikiwa unataka kuepuka umaskini, lazima uwe na nidhamu ya kutosha kufanya mambo ambayo si ya kufurahisha. Haifurahishi kusoma lakini ni lazima ufanye hivyo. Haifurahishi kuchukua hatua ambazo zinaweza kusababisha kushindwa lakini lazima ufanye hivyo. Kushindwa kunauma, lakini lazima uvumilie kushindwa na ujaribu tena. Kumbuka jinsi nilivyoanza makala hii; “Huwezi kupata matokeo mapya kwa kufanya mambo ya zamani na kila kitu kipya ni lazima kitakukosesha utulivu unapoanza kukifanya.” Kwa hivyo lazima uwe tayari kutoa sadaka ikiwa unataka kuepuka na kutokomeza umaskini na aibu zake zote.