Ushauri Bora Kutoka Kwa Rais Wa Zamani Wa Marekani Barack Obama Kwa Yeyote Anayetaka Kuwa Tajiri
Niliwahi kusoma nukuu iliyobadilisha maisha yangu. Nayo ilisema hivi: “Ikiwa unaweza kuishi miaka mitano ya maisha yako kwa njia ambayo watu wengine hawawezi kuishi, utafurahia maisha yako yote kwa njia ambayo watu wengi hawawezi.” Kwa sababu ya nukuu hii na msukumo mwingine mwingi nilioupata nilipoingia kwenye ulimwengu wa ujasiriamali nikiwa na umri wa miaka 21, sikuwa natarajia mafanikio ya haraka. Nilitarajia kushindwa kwa muongo mmoja na hiyo ndiyo sababu nimevumilia miaka hii migumu bila kulalamika au kutoa visingizio. Leo, nitashiriki nawe kile ninachokiona kuwa ushauri bora kutoka kwa Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama kwa kijana au mtu yeyote anayetaka kuwa tajiri.
Barack Obama alisema, “Kuacha alama yako duniani ni ngumu. Ikiwa ingekuwa rahisi, kila mtu angefanya hivo. Lakini siyo rahisi. Inahitaji uvumilivu, inahitaji kujitolea, na inakuja na kushindwa kwingi njiani.” Sikiliza, sababu ya watu wengi kuwa maskini si kwamba mfumo uliwadhulumu. Ni kwa sababu ni ngumu kuwa tajiri. Sababu ya ndoa nyingi kutofanya kazi si kwamba ni kawaida. Ni kwa sababu ni ngumu kudumisha muungano wenye furaha kati ya watu wawili. Sababu ya watu wengi kutofanikiwa maishani si kwamba kuna mtu aliwazuia. Ni kwa sababu ni ngumu, ni ngumu, na ni ngumu. Na watu wengi hawako tayari kupitia moto huo. Je, hii inakusaidiaje wewe msomaji wa Makala hii?
Kweli, kwa miaka mingi, nimegundua kwamba watu wengi hutoa visingizio na kulalamika kwa sababu wanatarajia maisha kuwa rahisi. Kwa mfano: Wako vijana wengi ni wahitimu wa chuo kikuu, umri wao ni kuanzia miaka 23 na zaidi ila pale wanapotaka kuanzisha biashara, lakini hawana pesa. Kwa hivyo wanailaumu serikali kwa kutowasaidia. Pole sana rafiki yangu kutoka chuo kikuu Mzumbe. Kitu kimoja natamani nikwambie ni hiki. “Ni Lazima ufanye kila uwezalo, anza kwa ugumu kadri uwezavyo, na pigana kwa bidii kadri uwezavyo.” Si rahisi. Ni kama nasikia ukisema Ndio. Naomba utambue ukweli mchungu kuwa haijawahi kuwa rahisi kwa yeyote. Kwa hivyo pigana kwa nguvu na akili zako mpaka mwisho hadi upate ushindi unaoutamani.
Kuna wewe mjasiriamali mwenye umri wa miaka 25, umeanzisha biashara yako kwa miaka mitatu na umepitia kushindwa kwingi. “Usilalamike. Bali endelea kupigana. Ni kawaida tu. Kila mtu ambaye amewahi kufanikisha jambo kubwa amepitia njia hiyo ngumu.” Na wewe mfanyakazi mwenye umri wa miaka 32 unaechukia kazi yako lakini unaogopa kitakachotokea ikiwa utafuata shauku yako ya muziki. Usijali kuhusu wewe mwenyewe. Najua kitakachokutokea. Utashindwa. Utashindwa na kushindwa mara nyingi. Hiyo ndiyo njia. Hiyo ndiyo njia inayoongoza watu kuelekea kwenye mafanikio halisi. Ni ngumu. Ni ngumu, ni ngumu. Na ndiyo maana ni watu wachache tu wanaoweza kufanikiwa au kuwa matajiri. “Kuacha alama yako duniani ni ngumu, ikiwa ingekuwa rahisi, kila mtu angefanya, lakini siyo rahisi. Inahitaji uvumilivu, inahitaji kujitolea na inakuja na kushindwa kwingi njiani.”
Winston Churchill alisema, “ikiwa unapitia jehanamu, endelea kwenda mbele.” Baada ya safari ndefu ya uhuru, baada ya Mandela kupigania uhuru wa watu wake kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na miaka mingi aliyotumia gerezani kama mfungwa, aliandika wasifu wake kwa jina, “The Long Walk to Freedom.” Kweli, vita vya maisha yake vilikuwa safari ndefu ya hofu. Pia, yako yatakuwa hivyo, ikiwa unataka kufanikiwa, kila safari ya mafanikio ni safari ndefu. Kama ingekuwa safari fupi, kila mtu angeifuata. Kama ingekuwa rahisi, kila mtu angeifanya.
Nimetenga miaka kumi mirefu ya maisha yangu kupigania uhuru wangu wa kifedha. Kutoka 2020 hadi sasa 2030. Hivi sasa 2024, miaka 4 ni kama 40/100. Nikwambie tu ukweli mpaka sasa safari hii siyo rahisi kama wengi wanavyofikriaa. Kuanguka au kushindwa ni kwingi sana. Kuna nyakati nililia sana. Nimepitia kukataliwa na kuvunjika moyo mara nyingi. Lakini sikurudi nyuma. “Katika nyakati zote ngumu sikurudi nyuma kwa sababu ilikuwa rahisi kuendelea mbele, lakini kwa sababu nilijua ugumu niliokuwa napitia ulikuwa wa kawaida kama kitu chochote.” Ikiwa unataka mafanikio ya kweli, usitarajie kuyapata kesho au kulala maskini ukaamka Tajiri kwa sababu ni safari ndefu na ngumu. Asante kwa kuambatana nami mpaka mwisho. Ubarikiwe!
Kutoka Elimika Fasta Academy, “Jifunze kwa Shauku, Ishi kwa Kusudi.” #PAMOJATUNASHINDA