Ushauri 10 kutoka kwa Warren Buffet kwa Vijana Wanaotaka Kuwa Matajiri
Warren Buffet, ambaye anachukuliwa kuwa mwekezaji tajiri zaidi kuwahi kuishi, alikua milionea mwaka 1960 akiwa na umri wa miaka 30 na tangu wakati huo, Buffet amekuwa mmoja wa watu matajiri zaidi duniani. Kwa miaka mingi, Warren Buffet ametoa ushauri mbalimbali kwa vijana kuhusu jinsi wanavyoweza kuwa matajiri na kufanikiwa. Katika makala hii, nitashiriki nawe ushauri 10 wa kuvutia zaidi kutoka kwa Warren Buffet. Ushauri namba 5 ni muhimu sana kwa hivyo unahitaji kusoma makala hii hadi mwisho.
Ushauri Namba 1: “Nitakuambia jinsi ya kuwa tajiri. Funga milango. Kuwa na hofu wakati wengine wanakuwa na tamaa. Kuwa na tamaa wakati wengine wanakuwa na hofu.” Kama kijana, ikiwa kuna ushauri wowote ambao unapaswa kuchukua kwa uzito kutoka kwa mtu yeyote, ushauri huo ni; Kuwa Tofauti. Nenda kinyume na mkondo. Tafuta kile ambacho kila mtu anafanya na ufanye kinyume chake. Lakini kwa nini hili ni muhimu?
Ni muhimu kufanya kinyume na kile ambacho kila mtu anafanya kwa sababu watu wengi duniani hawafikirii. Watu wengi duniani wanapata ugumu wa kutumia akili zao kwa hivyo mara nyingi kile wanachofanya kinaamuliwa na uthibitisho wa kijamii ambao kwa upande wake hufanya maamuzi yao kuwa mabaya. Kwa mfano, watu wengi watawekeza tu kwenye hisa wakati bei za hisa zinapanda kwa kasi, kwa bahati mbaya, hapo ndipo watu wenye akili wanauza. Ikiwa wewe ni wa kawaida, huwezi kufanikiwa. Usikubali kuwa wa kawaida! Tafuta kile ambacho kila mtu anafanya, na ufanye kinyume chake.
Ushauri Namba 2: “Haijalishi kipaji au juhudi ni kubwa kiasi gani, baadhi ya mambo yanachukua muda. Huwezi kumzaa mtoto kwa mwezi mmoja kwa kuwapa mimba wanawake tisa.” Unafikiri ni sababu gani kuu inayowafanya watu wengi duniani kuwa maskini na wasiofanikiwa? Ni kwa sababu, inachukua muda, kujitolea kwa hali ya juu na uvumilivu usio wa kawaida kutengeneza utajiri na kuyafikia mafanikio. Ni lazima uvumilie kwa subira nyakati ngumu au la sivyo huwezi kupitia barabara ngumu inayoelekea kwenye mafanikio yako. Mambo makubwa yanachukua muda. Huwezi kumzaa mtoto mwezi ujao kwa kuwapa mimba wanawake tisa leo.
Ushauri Namba 3: “Ni bora kuwa na watu bora kuliko wewe. Chagua marafiki ambao tabia zao ni bora kuliko zako na utaelekea katika mwelekeo huo.” Kitu kimoja ambacho vijana hufanya zaidi kuliko watu wa umri mwingine wowote ni kwamba, vijana hujumuika sana. Kwa bahati mbaya, watu wengi hawajui ni nani wanajumuika nao. Ebu fanya zoezi hili kabla ya kuendelea mbele zaidi. Fikiria na uorodheshe watu 5 ambao unatumia muda mwingi nao. Funga macho yako na fikiria hawa watu watakuwa wapi katika miaka 5 ijayo. Tambua pia, hapo ndipo unapoelekea. Hahahhaha. Ni rahisi sana. Ikiwa marafiki zako hawana malengo au hawana mtazamo mzuri kuhusu maisha, huwezi kuwa na mtazamo mzuri. Ikiwa marafiki zako hawajui zaidi yako, hutaweza kukua na kuwa mtu bora. Kwa hivyo unapaswa kufanya nini? Jitenge na watu hasi na wasio na motisha. Chagua marafiki zako kwa uangalifu kwa sababu huwezi kuwa bora kuliko wale unaojumuika nao.
Ushauri Namba 4: “Hutaweza kudhibiti muda wako, isipokuwa unaweza kusema ‘hapana.’ Huwezi kuruhusu watu wengine kuweka ajenda yako maishani.” Angalia karibu yako. Unaona nini? Vurugu. Vurugu. Vurugu kila mahali. Mitandao ya kijamii, TV, sherehe na sinema. Haya yote ni mambo ya kuvutia ambayo hayaleti thamani kubwa au kidogo kwa mtu anayetamani kuwa na maisha yenye tija. Kadiri tunavyoweza kusema “HAPANA” kwa vurugu, ndivyo tutakavyokuwa na muda mwingi wa kuwa na tija katika mambo ambayo ni ya muhimu kweli kweli.
Ushauri Namba 5: “Huna haja ya kuwa na akili zaidi kuliko wengine. Unahitaji kuwa na nidhamu zaidi kuliko wengine.” Sahau kila kitu ambacho umeambiwa kuhusu vipaji na IQ. Vipaji ni vya kawaida duniani kama chumvi ya mezani. Kuna mamia ya watu wenye alama za IQ 200 amabo ni maskini. Nidhamu, mazoezi, kujitoa na uvumilivu ndio unahitaji ili kufanikiwa.
Ushauri Namba 6: “Hatari inatokana na kutojua unachofanya.” Kwa mfano, zaidi ya 90% ya watu ambao wanapanga kuanzisha biashara zao wenyewe hawatachukua muda kusoma shule au kusoma hata vitabu 10 kuhusu biashara, sembuse 100, lakini, sote tunaamini kwamba biashara na uwekezaji ni hatari. Kwa nini wasiamini hivyo? Hatari halisi iko katika ujinga wako. Kadiri unavyojua zaidi kuhusu uwanja wako, ndivyo inavyokuwa hatari kidogo. Kupunguza hatari, tafuta maarifa.
Ushauri Namba 7: “Minyororo ya tabia ni nyepesi sana kuhisi hadi inapokuwa mizito sana kuvunjika.” Je, umewahi kuona mraibu wa dawa za kulevya akiwa hana msaada na akitamani nguvu fulani zimwokoe kutoka kwenye uraibu wake? Jambo bora unaloweza kufanya na maisha yako ni kuepuka tabia mbaya kabisa. Kucheza nazo ni kama kucheza na moto kwa sababu tabia zako mbaya zinapokua, unakuwa mtumwa wao.
Ushauri Namba 8: “Furahia kazi yako na ufanye kazi kwa wale unaowaheshimu.” Kulingana na utafiti wa Gallup Poll, 85% ya watu duniani kote wanachukia kazi zao. Kwa kuwa utatumia zaidi ya 50% ya maisha yako yote ya utu uzima ukifanya kazi na kupanga kufanya kazi, ni bora ufanye kila uwezalo kufanya kile unachofurahia. Inaweza kuwa si rahisi, lakini ikiwa utakuwa tayari kulipa gharama na kupitia maumivu muhimu, unaweza kujitengenezea aina ya kazi au biashara unayofurahia.
Ushauri Namba 9: “Huwezi kununua kilicho maarufu na kufanikiwa.” Hii ni sawa na hoja yetu ya kwanza. Unaona, wakati wowote kitu kinapokuwa maarufu, mchezo umekwisha. Iwe ni wazo la biashara au fursa ya uwekezaji. Unaposoma kuhusu hilo kwenye habari, ujue tayari umechelewa sana kuita fursa. Ukisisubri hadi itangaze na BBC au CNN ujue siyo fursa tena, ukicheza vibaya unakula za uso. Kitu halisi kiko kwenye siri. Kwa hivyo, unapataje fursa zilizofichwa ambazo hakuna mtu anaziona? Soma vitabu ambavyo hakuna mtu anayesoma. Tafuta maarifa wakati wengine wanatafuta burudani. Ikiwa unajua kile ambacho wengine hawajui, utaona fursa muda mrefu kabla hawajaona.
Ushauri Namba 10: “Usiwekeze katika biashara usiyoielewa.” Usiwe mtaalamu wa jumla. Kuwa mtaalamu. Chagua uwanja mmoja au kada unayopenda, soma kila siku kujua kile ambacho hakuna mtu anayejua kuhusu uwanja huo na sema “Hapana” kwa kitu kingine chochote usichokielewa. Ikiwa huwezi kuchukua muda kusoma biashara yoyote, usiwekeze kamwe kwa sababu kila mtu anafanya hivyo. Kwa mfano, usiwekeze kwenye Cryptocurrency kwa sababu tu kila mtu anafanya hivyo, ikiwa huwezi kuchukua muda kusoma kuhusu Cryptocurrency. Ni heri ukaacha kuweka hela yako huko au la sivyo tumia wataalamu wenye ujuzi na maarifa ya kutosha wakusaidie kuokoa fedha zako. Usiwekeze kwenye soko la hisa ikiwa huwezi kutengaa muda wako kusoma vitabu 10 vizuri kuhusu hisa. Usiwekeze katika mali isiyohamishika ikiwa huwezi kutumia muda wako kusoma angalau vitabu 5 vizuri kuhusu mali isiyohamishika. Tuma pesa zako tu pale ambapo maarifa yako yapo.
Kwa ufupi iko hivi, kama unataka kuwa tajiri, fanya kinyume na kile ambacho kila mtu anafanya, sema hapana kwa shughuli zisizo na tija, epuka tabia mbaya, chagua marafiki zako kwa uangalifu, kuwa na nidhamu na uvumilivu kwa sababu inachukua muda kufanikisha jambo lolote lenye thamani. Kutoka Elimika Fasta Academy, “Jifunze kwa Shauku, Ishi kwa Kusudi.” #PAMOJATUNASHINDA